Home Kaunti Familia ya Dedan Kimathi yaadhimisha miaka 103 tangu kuzaliwa kwake

Familia ya Dedan Kimathi yaadhimisha miaka 103 tangu kuzaliwa kwake

Evelyn Kimathi na Kanali Wambugu

Familia ya marehemu Dedan Kimathi mmoja wa waliopigania uhuru wa nchi hii imeadhimisha miaka 103 tangu kuzaliwa kwake wakati huu ambapo miito imetolewa kwa serikali ya Uingereza kusaidia kutambua eneo alikozikwa shujaa huyo wa uhuru.

Bintiye Kimathi kwa jina Everlyne Kimathi anasema mkinzano wa ziara ya Mfalme Charles wa 3 na mkewe malkia Camilla Parker nchini Kenya na siku ya kuzaliwa ya Kimathi ni ishara kwamba sasa ndio wakati mwafaka wa watu wa familia ya mfalme kusema jinsi watasaidia katika utambuzi wa kaburi la babake ili wampe maziko stahiki.

Alisema kama wakfu wa Dedan Kimathi waliamua kushirikiana na jeshi la Kenya KDF na wadau wengine kupanda miche ya miti ipatayo 100,000 katika eneo la karibu na bwawa la Sasumua huko Njabini Kinangop, kama sehemu ya mpango unaoendelea wa kuongeza ardhi ya misitu nchini.

Kanali Anthony Wambugu wa KDF alisema kwamba ushirikiano wao wa upanzi wa miti ni kuitikia wito wa amiri jeshi mkuu wa kuongoza katika upanzi wa miti bilioni 15 katika muda wa miaka 10 ijayo.

Aliomba jamii ya eneo la Njabini kutunza miche iliyopandwa ili kusaidia kuafikia lengo la serikali.

Mtunzaji wa misitu katika kaunti ya Nyandarua John Njoroge alisema kwamba huduma ya taifa ya misitu inatia bidii katika kuafikia idadi waliyopatiwa ya miti inayostahili kupandwa kote nchini.

Website | + posts
Lydia Mwangi
+ posts