Familia ya marehemu Agnes Wanjiru, aliyeuawa na mwanajeshi wa Uingereza mwaka 2012, inaendelea kutafuta haki, huku kamati ya bunge kuhusu ulinzi, ujasusi na uhusiano wa kigeni ikiimarisha uchunguzi wake kuhusu shughuli za kikosi cha wanajeshi wa Uingereza wanaofanya mazoezi hapa nchini (BATUK).
Uchunguzi huo unalenga kubainisha madai ya utovu wa nidhamu na ukiukaji wa haki za kibinadamu dhidi ya wanajeshi hao.
Alipofika mbele ya kamati hiyo ya bunge leo Jumanne, Esther Njoki Muchiri ambaye ni mpwa wa marehemu, alielezea kuhuzunishwa kwake kutokana na kucheleweshwa kwa uchunguzi huo.
“Tulijaza malalamishi yetu mwaka jana. Tuliitaka idara ya uchuguzi wa makosa ya jinai kutupatia majibu. Mbona swala hili linacheleweshwa?” aliuliza huku akitoa wito kwa kamati hiyo kuharakisha uchunguzi huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Nelson Koech, alitoa ahadi ya kuharakishwa kwa uchunguzi huo, wakati huo huo akimhakikishia Esther Wanjiru na mashirika ya kijamii kuwa kamati hiyo imejitolea kuhakikisha haki inapatikana.
Kamati hiyo imeandaa mikutano na wadau kadhaa, ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka shirika moja lisilo la iserikali, ambalo limedai kudhulumiwa na wanajeshi hao.
Shirika hilo limenakili visa kadhaa vya kudhulumiwa, kikiwemo kisa cha Robert Seuri, aliyefariki kutokana na kilipuzi na Lisoka Lessuyan, mtoto aliyepata majeraha mabaya kutokana pia na kilipuzi.
Wanachama wa kamati hiyo, awali waliandaa vikao vya kupokea maoni na malalamishi kutoka kwa umma katika kaunti za Laikipia, Isiolo, na Samburu mwezi Mei 2024 na kutathmini stakabadhi zilizowasilishwa na shirika hilo lisilo la kiserikali.
“Kile tunachohitaji ni kufidiwa kwa waathiriwa. Ni changamoto kwa kamati hii kubainisha kesi kuhusu marehemu Agnes Wanjiru,” alisema naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Bashir Abdullahi.
Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo, alisisitiza haja ya kupatikana kwa haki kwa waathiriwa wa visa vya dhuluma za kimapenzi vilivyohusishwa na wanajeshi hao wa Uingereza.
“Tunapaswa kubainisha matokeo ya visa hivyo. Kamati hii ipatiwe habari kuhusu kila kisa,” alisema Odhiambo.
Aidha kamati hiyo ilielezeea wasiwasi wake kuhusu maswala ya mazingira, yanayojumuisha utumizi wa silaha kama vile vilipuzi vya ardhini na kemikali aina ya phosphorous katika maeneo ya Llodaigia ambayo ni chemichemi ya maji na hushuhudia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Kamati hiyo itaendelea na uchunguzi wake, ikitarajiwa kuwahoji maafisa kutoka idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai DCI, halmashauri ya kitaifa ya usimamizi wa mazingira NEMA na wale wa huduma za wanyamapori DCI.