Home Habari Kuu Faith Kipyegon apatiwa tuzo ya juu zaidi ya Rais

Faith Kipyegon apatiwa tuzo ya juu zaidi ya Rais

0

Mwanariadha Faith Kipyegon ametunukiwa tuzo ya hadhi ya juu zaidi ya Rais inayojulikana kama “Elder of the Order of the Golden Heart of Kenya – EGH”.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya mwaka huu ya sikukuu ya Jamhuri katika bustani ya Uhuru, Rais Ruto alielezea kwamba tuzo hiyo ndiyo ya kiwango cha juu kabisa ambayo hutolewa kwa wananchi ambao huafikia ubora katika nyanja mbalimbali.

“Amejipatia nafasi kileleni kutokana na hatua yake ya kukimbia bila viatu na kuvunja rekodi mbili za dunia ndani ya mwaka mmoja na huo ndio ushujaa.” alisema kiongozi wa nchi akiongeza kwamba safari ya Faith ni msukumo kwa vijana na wanaotaka kuwa wanariadha.

Kipyegon ndiye mwanariadha pekee kati ya watu wote 27 waliotunukiwa hadhi hiyo leo kulingana na chapisho la gazeti rasmi la serikali la leo.

Wengine walio kwenye orodha hiyo ni mawaziri, magavana na viongozi wakuu serikalini.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Faith Kipyegon kushinda tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka kwenye tuzo za riadha ulimwenguni.