Mpango wa kuimarisha ubora wa majani chai, ni mkakati utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitano, kwa lengo la kuimarisha uzalishaji Majani Chai ambayo ni ya kumezewa mate, kutokana na ubora wake wa kiwango cha juu, na kupiga jeki ushindani uliopo katika sekta hiyo muhimu.
Mpango huo ulioanzishwa mwaka 2020, umetekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbali mbali wakiwemo wakuzaji wa majani chai, watafiti, wanunuzi, mawakala na viwanda vya kushughulikia majani chai.
Malengo makuu ya mpango huo ni pamoja na: Kubuni na kutekeleza mikakati ya kuinua na kuimarisha ubora wa majani chai katika mchakato wote wa ushughulikiaji zao hilo; Kuongeza maarifa na ujuzi kwa wanaozalisha majani chai kuhusu mbinu bora za ukuzaji, uvunaji na udhibiti wa ubora wa viwango.
Malengo mengine yanajumuisha kukumbatia teknolojia ya kisasa na mbinu bunifu katika uzalishaji majani chai, kutekeleza utafiti ili kufanikisha uteuzi wa aina bora za majani chai, udhibiti bora wa wadudu waharibifu na magonjwa.
Mengine ni usimamizi bora wa kuwezesha uteuzi wa mbinu bunifu; Kubuni na kutekeleza viwango vya ubora na sheria zinazoongoza sekta ya chai; Kuwezesha upatikanaji wa soko na kuhakikisha wateja wanapata bidhaa za majani chai za ubora wa hali ya juu.
Vigezo vingine katika mpango huo ni utoaji wa tuzo kwa kiwanda kitakachoibuka bora zaidi, kwa kuwa na Majani Chai ya ubora wa hali ya juu.
Viwanda ambavyo vimetambuliwa kuwa na Majani Chai ya viwango vya ubora wa chini, vitajumuishwa kwa mpango huo.
Bodi ya Majani Chai nchini, itatekeleza upimaji wa majani chai katika viwanda vya hapa nchini, shughuli itakayoongozwa na wataalam kutoka madalali na wauzaji wa zao hilo, ili kubainisha ubora wa majani chai ya Kenya, na kuziorodhesha kulingana na tathmini ya sampuli ya kila majani chai.
Hatua ya kutuza viwanda vya majani chai, inanuia kutoa motisha kwa viwanda hivyo kuhakikisha ubora wa juu wa majani chai ili kufanikisha upatikanaji wa bei bora za zao hilo.