Bodi ya Usimamizi katika Mamlaka ya Mawasiliano Nchini, CA imetangaza kwamba imekubali ombi la kujiuzulu kutoka kwa Ezra Chiloba.
Katika taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa bodi hiyo Mary Mungai, bodi hiyo imeelezea kwamba imekubali ombi hilo leo Oktoba 19, 2023.
Chiloba alimwandikia mwenyekiti wa bodi ya CA barua ya kujiuzulu Oktoba 18, 2023.
“Kwa niaba ya CA, namtakia Chiloba kila la kheri katika kazi zake za siku za usoni na kumshukuru kwa mchango wake maridhawa kwa mamlaka hii na katika sekta nzima ya mawasiliano nchini,” alisema Mungai.
Chiloba ambaye alikuwa amesimamishwa kazi kwa muda na bodi hiyo amekuwa akihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini kwa muda wa miaka miwili iliyopita.
Haya yanajiri yapata mwezi mmoja tangu bodi hiyo kutangaza uamuzi wa kumsimamisha kazi Chiloba na kumteua Christopher Wambua kumkaimu.
Kabla ya kujiunga na CA, Chiloba alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Mwaka 2020, Chiloba alisimamishwa kazi katika tume ya IEBC kutokana na maswali yaliyohusu manunuzi.