Timu za Ufaransa na Ureno zimeingia robo fainali ya mashindano ya bara Ulaya kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Ubelgiji na 3-0 dhidi ya Slovenia mtawalia. Bao la pekee la Ufaransa lillitiwa kimiani na Jan Vertonghen (aliyejifunga) mnamo dakika ya 85.
Ureno ilifunga mabao yake kupitia matuta ya penalti baada ya kutofungana kwenye muda wa kawaida na wa ziada. Katika ngarambe hiyo, nahodha Christiano Ronaldo alilia kwi kwi kwi alipopoteza mkwaju wa penalti waliozawadiwa baada ya Diego Jota kuchezewa visivyo.
Muda mfupi baadaye, aliyafuta machozi na kupachika wavuni tuta la kwanza. Bruno Fernandes na Bernard Silva walifunga la pili na tatu. Matuta matatu ya Slovenia yalipanguliwa na mlinda lango hodari Diogo Costa.
Ufaransa na Ureno sasa zitamenyana tarehe tano saa nne usiku.
Leo Jumanne ni mwisho wa hatua ya mwondoano. Romania itakwaruzana na Uholanzi saa moja usiku kisha Uturuki ikabane na Austria saa nne usiku.