Home Burudani Esma Platnumz afunga ndoa kwa mara nyingine

Esma Platnumz afunga ndoa kwa mara nyingine

0

Dada ya mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Bongo Flava nchini Tanzania Diamond Platnumz, Esma Platnumz ameolewa kwa mara nyingine.

Esma alifunga ndoa na meneja wa wasanii wa muziki Rashid Shaibu maarufu kama Jembe One katika hafla ya kufana kwenye msikiti wa Masjid Akram, Mbezi Beach Februari 22, 2024 jioni.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na jamaa na marafiki wa wawili hao na hii ni ndoa ya tatu anaingia Esma baada ya kuolewa na Petit Man Septemba 2014 na mfanyabiashara Yahya Msizwa Julai 2020.

Wakosoaji mitandaoni wanahisi kwamba huu ni upepo wa kupita haraka ikitizamiwa kwamba Esma ameshakuwa kwenye ndoa za awali ambazo hazikudumu na hii ya sasa anamzidi umri mume wake.

Esma na Jembe One baada ya kufunga ndoa

Kupitia mitandao ya kijamii, Esma alielezea jinsi yeye na Jembe One walikutana akisema kwamba Jembe alimwalika nyumbani kwake kupitia ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

Anasema hakuwa na sababu ya kukosa kuitikia mwaliko huo wa kumzuru Jembe nyumbani kwake na alipofika huko aliridhishwa na mandhari na mapishi ya mwenyeji wake.

Kulingana naye, mvuto huo ulisababisha akae huko kwa Jembe One kwa muda wa siku tatu na hapo ndipo mapenzi yao yaliota.