Home Burudani Eric Omondi amhamisha na kumfungulia biashara Victor Juma

Eric Omondi amhamisha na kumfungulia biashara Victor Juma

0

Mchekeshaji Eric Omondi amemhamisha jamaa kwa jina Victor Omondi na familia yake kutoka mtaa wa Mathare na kumfungulia biashara ya kuuza viatu na nguo. Amesema duka hilo litazinduliwa rasmi kesho Jumanne.

Juma alipata kujulikana baada ya kukamatwa wakati wa maandamano mtaani Mathare na afisa wa polisi ambaye alikuwa akijisingizia kuwa mwanahabari.

Kwenye video iliyosambazwa mitandaoni ya tukio hilo, Victor alisikika akilalamikia maafisa wa polisi kwa kurusha vitoa machozi ambavyo vilisababisha mtoto wake kuzirai.

Omondi alimfuata Juma hadi mahakamani alikoachiliwa huru. Baadaye, aliandaa mchango kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii akisema alitaka kubadilishia maisha baba huyo wa mtoto mmoja.

Alifanikiwa kuchangisha shilingi laki 4 ambazo alisema zitatumika kulipia ada za hospitali za familia hiyo, kufungua biashara ya viatu na nguo, kumfungulia mkewe Juma mkahawa mdogo, kulipa ada ya nyumba ya mwaka mzima na kulipa ada ya shule ya chekechea ya mwanao kwa muda wa miaka miwili.

Aliahidi pia kumtangazia biashara yake kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii jambo ambalo amesema linaanza mara moja.

Omondi alisema watanadi mali iliyoko kwenye duka jipya la Juma mubashara kwenye mitandao ya kijamii na ikiisha ataagiza nyingine na watauza vivyo hivyo hadi pale ambapo Juma ataweza kujisimamia kama mfanyabiashara.

Eric Omondi amekuwa akitumia ufuasi wake mkubwa mitandaoni kuchangisha pesa za kusaidia waathiriwa wa maandamano.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here