Bei za mafuta hazijaongezwa kwenye tathmini ya kila mwezi ya Halmashauri ya Kudhibiti Bei za Nishati na Mafuta, EPRA.
Hii inafuatia tangazo la juzi Jumapili usiku la Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo Daniel Kiptoo.
“Ili kuwakinga wateja dhidi ya bei ya juu ya mafuta, serikali imeamua kudhibiti bei za mafuta katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba,” ilisema taarifa ya EPRA.
Lita moja ya petroli itaendelea kuuzwa kwa shilingi 194 na senti 68 jijini Nairobi, dizeli shilingi 179.67 nayo mafuta taa shilingi 169.48.
Jijini Mombasa, waendeshaji magari wataendelea kununua lita moja ya petroli kwa shilingi 191.62, shilingi 176.63 kwa lita ya dizeli na shilingi 166.43 kwa lita ya mafuta taa.
Bei hizo zitasalia hivyo hadi Septemba 14.
Kiptoo amesema wauzaji mafuta watafidiwa tofauti ya bei kutoka kwa hazina ya ustawishaji mafuta kwa kiwango cha shillingi 7.33 kwa lita ya mafuta ya petroli, shillingi 3.59 kwa lita ya dizeli na shilingi 5.74 kwa lita ya mafuta taa.