Home Kimataifa Enrique Tarrio ahukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani

Enrique Tarrio ahukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani

0
Enrique Tarrio

Aliyekuwa kiongozi wa kundi la “Proud Boys” Enrique Tarrio alihukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani Jumanne Septemba 5, 2023, kutokana na jukumu lake la kupanga wafuasi wa aliyekuwa Rais Donald Trump kushambulia majengo ya Capitol Januari 6, 2021.

Kifungo chake ndicho kirefu zaidi kilichotolewa dhidi ya wahusika wa vurugu za Januari 6 kufikia sasa.

Upande wa mashtaka ulikuwa unataka ahukumiwe kifungo cha miaka 33 gerezani kwa kile ambacho walikitaja kuwa hatua ya Tarrio na wanachama wengine watatu wa kundi la Proud Boys kutumia nguvu kupita kiasi kujaribu kulazimisha viongozi waliochaguliwa kukubali mtazamo wao wa kisiasa na kubadilisha majibu ya uchaguzi.

Mawakili wa Tarrio hata hivyo walimtetea wakisema anastahili hukumu nafuu kwa sababu alishirikiana na maafisa wa usalama katika uchunguzi wa siri kuhusu madawa ya kulevya baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ulaghai na kwa sababu hali yake ya afya ya akili imedhurika wakati akiwa kizuizini.

Tarrio hakuwepo kwenye vurugu za Capitol Januari 6, 2021 kwa sababu alikuwa amekamatwa siku mbili kabla ya tukio hilo lakini viongozi wa mashtaka wanaamini alipanga na kuelekeza shabulizi hilo.

Jaji Timothy J. Kelly alisema Tarrio alikuwa amefanya kosa kubwa, ni aliongoza njama hiyo na anamotishwa na ari ya mapinduzi.