Home Habari Kuu Eneo la Magharibi laathiriwa zaidi na mafuriko

Eneo la Magharibi laathiriwa zaidi na mafuriko

0

Eneo la magharibi mwa nchi ndilo limeathirika zaidi na mvua ya masika ya mwezi Machi hadi Mei, hususan maeneo yaliyo karibu na Ziwa Viktoria na maeneo ya milima mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa.

Haya ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali Isaac Mwaura aliyezungumza wakati wa kutoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya mafuriko nchini katika jumba la Nyayo jijini Nairobi.

Alisema Ziwa Viktoria limejaa kabisa halina nafasi ya maji zaidi lakini vyanzo vya maji havikomi kutiririsha maji yake humo na maji ya ziada yamefurika katika makazi ya watu.

Mashamba, maeneo ya kupokea samaki baada ya uvuvi na maeneo mengine pia yameathiriwa na mafuriko hayo.

Shughuli za kila siku za wakazi wa maeneo hayo zimetatizwa na hali inatizamiwa kuzorota zaidi kabla ya kuanza kuimarika kulingana na Mwaura.

Serikali inapanga kusaidia watu wapatao elfu 40 ambao tayari wamehisi athari za mafuriko hayo na wale ambao wako katika hatari katika eneo la Nyanza.

Mwaura alizuru eneo hilo ili kujifahamisha kuhusu hali ilivyo na kuongoza mipango ya serikali ya usaidizi. Alikuwa ameandamana na mrakibu wa eneo la Nyanza Flora Moroa, katibu mkuu wa shirika la msalaba mwekundu Idris Ahmed, Kamishna wa kaunti ya Kisumu na viongozi wengine.

Familia 408 zilipokea msaada wa chakula na vifaa vingine katika shule ya upili ya Nduru huku serikali ikiendelea kupanga kutoa shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya athari za mafuriko.