Home Burudani Embarambamba na Getumbe watakiwa kuondoa nyimbo zao “chafu” mitandaoni

Embarambamba na Getumbe watakiwa kuondoa nyimbo zao “chafu” mitandaoni

0

Bodi ya kuorodhesha filamu nchini KFCB imetangaza kwamba imetuma nyaraka kwa wasanii Chris Embarambamba na William Getumbe kuwaelekeza waondoe video za nyimbo zao chafu kwenye mitandao ya kijamii.

Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Nelly Muluka, nyimbo hizo zimesingiziwa kuwa za injili lakini zinaletea aibu dini ya kikristo.

Embarambamba alitoa wimbo uitwao “Niko Uchi” huku Getumbe ambaye anasemekana kuwa mhubiri akitoa wimbo uitwao “Yesu Ninyandue”.

Muluka kwenye taarifa hiyo alisema kwamba wawili hao wameagizwa kufuta kazi hizo za sanaa mitandaoni la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Majukwaa ya mitandaoni pia yaliandikiwa barua za kuomba kufuta kazi hizo chafu.

Wakati huu ambapo wanafunzi wanarejea nyumbani kwa likizo fupi ya katikati ya muhula, Muluka anahisi kwamba nyimbo na video kama hizo zenye jumbe potovu huenda zikapotosha watoto hao.

Alitaja pia video iliyosambazwa ya mhubiri kwa jina Askofu Johanna ambaye alionekana kwenye video akimshika mwanamke fulani kwa njia isiyo nzuri kwa madai ya kumwondolea mapepo.

Shirika la kusimamia hakimiliki za muziki nchini MCSK pia limetangaza kwamba limeanzisha mchakato wa kuondoa majina ya Embarambamba na Getumbe kwenye orodha ya wasanii.

Mkurugenzi mtendaji wa MCSK Daktari Ezekiel Mutua alisema kwamba iwapo sera iliyopitishwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka itaanza kutumiwa, wawili hao hawatapata mirahaba kwa miaka mitano.

“Wakirudia makosa yao watakuwa katika hatari ya kupigwa marufuku kabisa.” aliandika Mutua akisema ni sharti maadili yadumishwe.

Website | + posts