Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imefutilia mbali ugawaji haramu wa kipande cha ardhi cha ekari 18 ambacho kilikuwa kimenyakuliwa na mtu binafsi katika kaunti ya Kisumu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak amesema mtu ambaye alidai kumiliki ardhi ya soko hilo alijaribu kuiuza kwa serikali ya kaunti hiyo kwa bei ya juu zaidi, hali iliyomfanya Gavana wa kaunti hiyo Prof. Anyang’ Nyong’o kutafuta usaidizi wa tume hiyo.
Akiandamana na Prof. Nyong’o, Mbarak alisema tume hiyo inashirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti ya Kisumu kwa lengo la kurejesha mali nyingine iliyonyakuliwa katika kaunti hiyo, zikiwemo nyumba na maeneo yaliyotengewa ujenzi na upanuzi wa barabara.
Alisema EACC imetwaa na kurejesha mali za idara ya mahakama huko Kisumu, mali za shirika la reli nchini na mali za hifadhi ya taifa, zote za thamani ya shilingi bilioni tatu huku akiwataka wananchi kushirikiana kwa karibu na tume hiyo.
Aliyasema hayo alipowahutubia wafanyabiashara waliokuwa na furaha katika soko la Kibuye.
Kwa upande wake, Prof. Nyong’o, alishukuru tume hiyo na ile ya kitaifa ya ardhi kwa kuwezesha kutwaliwa kwa ardhi ya umma iliyokuwa imenyakuliwa.
“Ninashukuru EACC na Tume ya Taifa ya Ardhi kwa kutusaidia kupata ardhi iliyokuwa imenyakuliwa katika kaunti hii, huku tunapoorodhesha ardhi na mali iliyonyakuliwa na kutoa ilani kwa wanaozimiliki,” alisema Gavana Nyong’o.