Home Habari Kuu EACC: Kaunti ya Busia ndio fisadi zaidi nchini

EACC: Kaunti ya Busia ndio fisadi zaidi nchini

0

Kaunti ya Busia imeorodheshwa kuwa fisadi zaidi nchini.

Hii ni kulingana na ripoti ya Kitaifa kuhusu Ufisadi (NEC) 2023 iliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) leo Jumatano.

Ripoti hiyo ilifichua kuwa ukitafuta huduma katika kaunti, lazima utatoa hongo ili uhudumiwe.

Kulingana na EACC, kaunti tano za kwanza ambazo ufisadi umekithiri zaidi ni Busia, Baringo, Nairobi, Nakuru na Machakos.

Ukitaka kuhudumiwa kwenye kaunti ya Busia, utaulizwa kutoa hongo mara 2.02, Baringo mara 1.34, Nairobi (1.12), Nakuru (1.11) na Machakos (1.09).

Kaunti tano zilizo na visa vya ufisadi kwa kiwango cha chini ni Nandi mara 0.50, Nyeri (0.49), Vihiga (0.47), Embu (0.43) na Lamu (0.40).

Aidha, kaunti tano za Nyamira, Baringo, Siaya, Bungoma na Turkana, anayetaka huduma lazima atoe hongo asilimia 100. Kaunti ambazo utapata huduma bila kutoa hongo ni Taita Taveta (48%), Vihiga (47%), Mandera (46%), Embu (44%) na Nyeri (40%).

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kaunti ya West Pokot inaongoza kwa kiasi cha pesa ambazo utatoa kwa hongo ikiwa ni shilingi 56,695 ikifuatwa na Nairobi (Ksh 37,768), Murang’a (18,378), Kisii (Ksh16,810), Uasin Gishu (Ksh10,136) na Kitui (Ksh9,849).

Utoaji wa hongo kwenye kaunti ya Kilifi upo chini ambapo utalipia shilingi 162 ikifuatwa na Tana River (Ksh 505), Kakamega (Ksh 538), Kericho (Ksh 681) na Marsabit (Ksh 902).

Ufisadi uliorodheshwa katika nafasi ya nne kwa matatizo makubwa yanayokabili nchi baada ya gharama kubwa ya maisha, ukosefu wa ajira na umaskini.

Kwa jumla, 34.4% ya waliotafuta huduma za serikali waliombwa kutoa hongo huku 28.3% wakilipa.

Alphas Lagat
+ posts