Home Biashara Duale: Kiwanda cha KMC kitaimarishwa kuwa bora zaidi

Duale: Kiwanda cha KMC kitaimarishwa kuwa bora zaidi

Duale amehimiza uongozi wa kiwanda hicho kuwa na uvumbuzi zaidi, ili kuhakikisha wanakusanya mapato zaidi na wakati huo huo kukata matumizi yasiyofaa.

0
Waziri wa Ulinzi Aden Duale azuru kiwanda cha utayarishaji nyama cha KMC.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale amesema wizara ya ulinzi imejitolea kubadilisha kiwanda cha kutayarisha nyama nchini KMC, kwa nia ya kukiwezesha kuimarisha utayarishaji wa nyama za ubora wa hali juu.

Duale alisema kwamba serikali ya Kenya kwanza imeazimia kubadilisha sekta ya kilimo katika uzalishaji wa mazao na mifugo ili kuboresha mapato ya wakulima kote nchini.

Akiongea katika makao makuu ya kiwanda hicho eneo la Athi River wakati wa kutia saini mkataba wa kandarasi ya utendakazi kati ya kiwanda hicho na wizara ya ulinzi, waziri huyo alisema kwa miaka mingi, wizara hiyo imekuwa ikijulikana sana kwa uadilifu, ufanisi, weledi na matumizi ya busara ya rasilimali za umma na kwamba maadili sawa yatapitishwa kuendesha kiwanda hicho.

Aidha waziri huyo alipongeza uongozi wa kiwanda cha KMC, kwa kufanyia mabadiliko kiwanda hicho katika kipindi cha muda mfupi, akisema mengi yanahitaji kufanywa ili kurejesha imani ya wakulima.

“Nilikuwa hapa miaka kadhaa iliyipota lakini kiwanda hiki kimebadilika. Haya ni mabadiliko ya kumezewa mate. Nawapongeza viongozi wa kiwanda hiki kwa mabadiliko hayo,” alisema waziri huyo.

Duale amehimiza uongozi wa kiwanda hicho kuwa na uvumbuzi zaidi, ili kuhakikisha wanakusanya mapato zaidi na wakati huo huo kukata matumizi yasiyofaa.

Tangu kiwanda hicho kuwekwa chini ya wizara ya ulinzi, zaidi ya mifugo 50,000 wamechinjwa na wakulima kulipwa shilingi milioni 2.2 katika kaunti 37.