Home Habari Kuu Dorcas Rigathi: Ipo haja ya kuangazia haki za mtoto wa kiume

Dorcas Rigathi: Ipo haja ya kuangazia haki za mtoto wa kiume

Mke wa naibu rais mhubiri Dorcas Rigathi ametoa wito kwa viongozi wakiwemo wale wa kidini kuangazia maslahi ya mtoto wa kiume na vijana.

Dorcas alisema hatma ya taifa hili inaangazia kumuokoa mtoto wa kiume kuepuka tabia potovu kama vile uraibu wa mihadarati na pombe.

Mchungaji huyo alisikitika kwamba visa vya utumiaji dawa za kulevya na ubugiaji pombe vimeongezeka mno katika miaka ya hivi punde, hali ambayo imeathiri maisha ya mtoto wa kiume.

Aidha, alikariri kuwa msingi na usalama wa familia haviwezi kudumishwa ipasavyo ikiwa watoto wavulana watapuuzwa.

Alikuwa akiongea wakati wa mafunzo kwa viongozi 1,000 wa kidini kutoka kaunti zote 47 kuhusu jinsi ya kushughulikia changamoto za UKIMWI, utumiaji dawa za kulevya na pombe miongoni mwa wavulana na wanaume hapa nchini..

Wakati uo huo, alisema ukosefu wa ulezi wa baba unaohitajika na kusambaratika kwa familia vimemuathiri mtoto wa kiume na kumwacha bila mshauri.

Aidha alidokeza kuwa  wakati umewadia wa kubuni sera na mikakati itakayomwezesha mtoto mvulana, mbali na kuwarekebisha wale waliopotoka.

Website | + posts
feedback@kbc.co.ke | Website | + posts