Home Kimataifa Dorcas Oduor: Nitazitathmini kesi kwa makini kabla ya kuziwasilisha kortini

Dorcas Oduor: Nitazitathmini kesi kwa makini kabla ya kuziwasilisha kortini

0
kra

Dorcas Oduor ambaye ameteuliwa na Rais William Ruto kuwa Mwanasheria Mkuu amesema utakuwa wajibu wake kuzitathmini kwa makini kesi kabla ya kuziwasilisha mahakamani. 

Matamshi yake yanawadia wakati ambapo serikali imekuwa na hulka ya kupoteza kesi nyingi zilizowasilishwa mahakamani, ya hivi karibu ikiwa rufaa iliyowasilishwa dhidi ya Mswada wa Fedha 2023.

kra

Oduor amesema hatua hiyo itasaidia kuepusha serikali kukumbwa na hasara kubwa zinazotokana na kupoteza kesi zinazowasiliswa mahakamani.

“Itakuwa pia kazi yangu kuzishauri wizara, idara na mashirika kuhusu namna ya kushughulikia kesi mahakama,” alisema Oduor leo Ijumaa wakati akisailiwa na kamati ya bunge kuhusu uteuzi inayoongozwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula.

Alipoulizwa ni kwa nini licha ya kuwa na utendakazi wa kupigia mfano na kuelimika ipasavyo, hajafanikiwa kujiunga na idara ya mahakama licha ya kutuma maombi ya kutaka kuwa Jaji, Oduor alisema aliamini hakufanikiwa kwa sababu wakati wake haukuwa umewadia.

Ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa, Oduor atakuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu nchini.

Wadhifa huo uliachwa wazi kufuatia kuteuliwa kwa Justin Muturi kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma.

Awali, ulikuwa umekabidhiwa Rebecca Miano, lakini uteuzi huo ulibatilishwa na Miano kuteuliwa kuwa Waziri wa Utalii.

Awali, kamati ya bunge juu ya uteuzi ilimsaili Beatrice Askul Moe aliyeteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

 

 

Website | + posts