Home Taifa Dereva Ian Njoroge afikishwa kortini kwa kushambulia polisi

Dereva Ian Njoroge afikishwa kortini kwa kushambulia polisi

0

Ian Njoroge ambaye ni dereva wa matatu aliyenaswa kwenye video akimshambulia polisi amefikishwa mahakamani leo Jumanne asubuhi. 

Mbugua alikamatwa na polisi baada ya kuonekana kwenye video hiyo iliyosambazwa mno mitandaoni akimpa afisa wa polisi kichapo cha mbwa kwenye barabara ya Mirema, Roysambu jijini Nairobi.

Wakati wa tukio hilo, mshtakiwa alionekana kuwa mwenye ghadhabu tele huku akimshambulia afisa huyo kwa makofi na mateke hadi akamuangusha mtaroni.

Njoroge alikamatwa kwenye makazi yake katika eneo la Jacaranda, Kayole kaunti ya Nairobi juzi Jumapili usiku kwenye operesheni iliyoongozwa na maafisa wa upelelezi wa jinai, DCI.

Baadaye, video ilichapishwa mtandaoni ikimwonyesha Njoroge akiwa amefungwa pingu huku akihojiwa na maafisa wa polisi. Akijitetea, dereva huyo ameripotiwa kudai kwamba afisa huyo aliitisha kiasi kikubwa cha hongo kilichomfanya damu kuchemka na kuamua kumshambulia.

Kisa hicho kilizua gumzo katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya Wakenya wakimhurumia dereva huyo wakisema atatumiwa na maafisa wa polisi kama onyo kwa yeyote anayepanga kushambulia afisa wa polisi.

Website | + posts