Mwimbaji wa nyimbo za injili Dennis Njoroge maarufu kama Denno anaadhimisha miaka 15 tangu kujiunga na tasnia ya muziki.
Denno ambaye hana uwezo wa kuona aliandaa tamasha la shukrani na kusherehekea muda wake katika sekta ya muziki wa injili katika ukumbi wa Talanta huko Ongata Rongai, kaunti ya Kajiado Jumamosi Julai 8, 2023.
Waimbaji wenzake kama vile Daddy Owen, Kambua, Harry Richie na Jacque JC walihudhuria hafla hiyo.
Mgeni wa heshima kwenye hafla hiyo alikuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la hakimiliki za muziki nchini MCSK Daktari Ezekiel Mutua ambaye alimpongeza Denno kwa muda ambao amekuwa akimtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji. “Naomba mwenyezi Mungu akuinue zaidi. Umeshinda kikwazo cha kutokuwa na uwezo wa kuona, ukapata kutambulika katika tasnia ya muziki na sasa umechukua hatua ya kushauri wasanii wanaoibuka.” aliandika Mutua kwenye Facebook.
Kambua alichapisha picha kwenye Insta Stories akiwa jukwaani na Daddy Owen na Denno kwenye hafla hiyo akisema alipitia huko.
Akizungumza kwenye mahojiano na wanahabari wa mitandaoni, Denno alielezea kwamba yeye kama msimamizi wake wa awali Bahati aliwaza kuacha kuimba nyimbo za injili na kuingilia muziki wa dunia. Alitaja mwanamuziki Nyashinski ambaye anaimba nyimbo za dunia akisema huwa analipwa pesa nyingi.
Alishukuru usimamizi wake wa awali wa kampuni ya EMB ya mwanamuziki Bahati akisema yeye ndiye msanii pekee aliyetoka huko na gari hata kama alikaa huko miezi 8 pekee.