Home Habari Kuu DCI yawatahadharisha wahudumu wa teksi dhidi ya wahalifu

DCI yawatahadharisha wahudumu wa teksi dhidi ya wahalifu

0
Wahudumu wa teksi watakiwa kuwa macho dhidi ya wahalifu.

Idara ya upelelezi wa jinai DCI, imewataka wahudumu wa teksi kuwa waangalifu kufuatia ongezeko la makundi ya uhalifu yanayowalenga. 

Katika taarifa kupitia mtandao wa X, idara hiyo ilieleza kuwa makundi hayo hutumia ujanja, ambapo hujisingizia kuwa wateja wanaotafuta huduma za teksi kwa safari za masafa marefu au kupitia sehemu mbalimbali wakiwabeba wenzao kabla ya kuwaibia madereva magari na mali yao.

DCI ilisema wahuni hao hukubaliana na mhudumu wa teksi kuhusu malipo, huku wakiahidi kuongeza fedha kwa sababu ya kubadili mkondo ili kusimama kuwachukua wenzao.

Katika tukio la hivi majuzi lililoripotiwa katika kituo cha polisi cha Kikopey mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru mwezi jana, mhudumu mmoja wa teksi mwenye umri wa miaka 42 kutoka Nairobi, alitakiwa kumpeleka mteja mmoja hadi Nakuru, lakini aliibiwa gari lake na kuachwa katika eneo la Diatomite.

Baada ya kupashwa habari, kundi la maafisa wa DCI kutoka makao makuu, lilitumwa kuwasaka washukiwa hao, ambapo wawili kati yao walikamatwa.

Wawili hao waliotambuliwa kuwa Francis Ojerepata Omoindi mwenye umri wa miaka 39  na Jack Odhiambo Otieno  mwenye umri wa miaka 38, walikamatwa katika kaunti ya Bungoma.

Gari lililoibwa, kadi wia 7, vitambulisho 5 na leseni mbili za kuendesha magari  zilipatikana kutoka kwa washukiwa hao.

Kesi hiyo inaendelea katika mahakama moja ya Naivasha, huku uchunguzi dhidi ya washukiwa wengine ukiendelea.