Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI jijini Mombasa anataka wanaume wawilii kuzuiliwa kwa kipindi cha wiki tatu ili kubaini mmiliki wa bangi yenye thamani ya shilingi milioni 9.4. Bangi hiyo ilipatikana ikiwa kwenye gari lililoachwa aina ya Toyota Land Cruiser katika eneo la Kanamai, kaunti ya Kilifi.
Hii ni baada ya gari hilo lililotumiwa kusafirisha bangi hiyo kubingiria kwenye mtaro Septemba 4 mchana.
Gari hilo ambalo tairi yake ya nyumba ilipata pancha linaaminika kuendeshwa kwa kasi zaidi wakati lilipoondoka barabarani na kubingiria mtaroni.
Waliokuwamo walitimka mbio na kutoroka punde baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Katika ombi lao kwa Hakimu Mkuu Mkazi Yusuf Shikanda, DCI inasema wamechukua alama za vidole kwenye gari hilo kwa lengo la kubaini mmiliki wake.
DCI imetaka kukubaliwa kuwazuia Mughanga Ruwange na Dennis Shere kwa tuhuma za kushirikiana na mmiliki wa gari hilo lililokuwa likisafirisha bangi hiyo yenye thamani ya mamilioni ya pesa.
Washukiwa hao wawili walikamatwa nyumbani kwao katika eneo la Kanamai Majengo kaunti ya Kilifi Septemba 12.
Hata hivyo, wawili hao kupitia mawakili wao Julius Ireri na George Anango walipinga kuzuiliwa kwao kwa siku 21 ili kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi kufanyika.
Waliiambia mahakama kuwa polisi hawana ushahidi unaowahusisha na bangi hiyo.
Washukiwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mtwapa huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi juu ya ombi la DCI la kutaka kuwazuilia Jumatatu wiki iijayo.