Home Habari Kuu COWU yamtaka Rais Ruto kushinikiza kulipwa kwa madeni ya shirika la Posta

COWU yamtaka Rais Ruto kushinikiza kulipwa kwa madeni ya shirika la Posta

Posta iliyo na wafanyikazi takriban 2500 hutumia shilingi milioni 131 kila mwezi kulipia mishahara ya wafanyikazi hao.

0

Muungano wa wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano nchini, COWU umemtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kushinikiza kulipwa kwa madeni ambayo shirika la Posta nchini linadai mashirika yaliyopokea huduma zake.

Kulingana na katibu mkuu wa COWU Benson Okwaro, shirika la Posta linadai shilingi zaidi ya bilioni 3 ambazo zinatosha kulipa wafanyakazi 2,500 wa shirika hilo malimbikizi ya mishahara ya miezi minne.

Kulingana na Okwaro, tume ya IEBC inadaiwa na Posta shilingi bilioni 1.1,Huduma Centres shilingi bilioni 1.8 na KENHA shilingi milioni 53.

Wafanyakazi wa Posta hawajalipwa mshahara tangu mwezi Mei mwaka huu.

“Kile tunamwomba Rais ni kushinikiza wadeni wote wa Posta waliopokea huduma kulipa na wakifanya hivyo Posta itapata zaidi ya shilingi bilioni tatu ambazo zinatosha kulipa malimbikizi yote ya mishahara na hata madeni yake mengine,” alisema Okwaro.

”IEBC inadaiwa na Posta shilingi bilioni 1.1 kutoka kwa uchgauzi mkuu wa mwaka uliopita na kuna KENHA inayodaiwa shilingi milioni 53 na Huduma Centres wakilipa posta kodi wanayodaiwa ya shilingi bilioni 1.8 zitatosha kumaliza shida zote za shirika la Posta.”

Shirika hilo lililo na wafanyakazi takriban 2,500 hutumia shilingi milioni 131 kila mwezi kulipia mishahara ya wafanyakazi hao.