Home Habari Kuu COWU yaiomba serikali isaidie kampuni ya Telkom

COWU yaiomba serikali isaidie kampuni ya Telkom

0

Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano Nchini, COWU kimeiomba serikali isaidie kampuni ya Telkom isije ikafilisika.

Katibu Mkuu wa chama hicho Benson Okwaro anasema kampuni hiyo inakumbwa na madeni mengi na huenda ikafungwa hivi karibuni na kusababisha wengi kupoteza ajira.

Haya yanajiri baada ya kampuni iitwayo American Towers Corporation (ATC) kuzima mitambo ya kurusha na kupokea mawimbi ya huduma za Telkom kote nchini kufuatia deni la shilingi milioni 200.

Mwaka 2013, Telkom iliuzia ATC vituo vyake 723 kwenye mkataba ulionuiwa kupunguza gharama ya kufanya biashara.

Kulingana na Okwaro, hatua ya Telkom ya kuuza vituo hivyo haikuwa nzuri na ndiyo chanzo cha masaibu yake.

Alielezea kwamba mitambo hiyo awali ilikuwa ikimilikiwa na Telkom ambayo iliiuza kwa ATC na sasa lazima iikomboe kutoka kwa ATC kwa matumizi.

Okwaro anahisi kwamba ikiwa tatizo lililopo litakithiri, kampuni ya Telkom itashindwa kulipa wafanyakazi wake wapatao 600 na kugharimia shughuli zake.

Wastaafu elfu 6 wa lililokuwa shirika la Posta pia wako kwenye hatari ya kukosa malipo yao ya uzeeni.

Mfumo wa mawasiliano ya kukusanya taarifa za ulinzi pia uko hatarini kwani umesimikwa kwa kampuni ya Telkom na hivyo lazima serikali iwajibike.

Katibu huyo wa COWU anapendekeza kwamba serikali iipatie Telkom shilingi bilioni 6 na itafute njia za kuiwezesha kupata faida.

Anapendekeza pia kwamba serikali ilipe deni la Telkom la shilingi bilioni mbili kama njia ya kuisaidia kugharimia shughuli zake.

COWU inataka uchunguzi kamili ufanyike kuhusu ubadilishanaji wa umiliki wa kampuni ya Telkom na mali zake kwani nyingi ya mali hizo zimeuzwa kwa watu na kampuni binafsi kwa njia isiyo halali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here