Home Habari Kuu Chuo Kikuu cha Moi chasitisha safari za masomo kwa muda

Chuo Kikuu cha Moi chasitisha safari za masomo kwa muda

0

Chuo Kikuu cha Moi kimefutilia mbali kwa muda safari za kimasomo kufuatia ajali ya basi iliyotokea leo Jumatano asubuhi.

Basi hilo lililokuwa limewabeba wanafunzi 65 likielekea Mombasa lilipata ajali eneo la Kimende kwenye barabara ya Nakuru kuelekea Nairobi.

Naibu Chansela Isaac Kosgei alitangaza hayo kupitia taarifa akisema safari hizo zitarejelewa baada ya likizo ya Pasaka.

“Takriban saa 3:50 asubuhi ya leo, basi letu la Chuo Kikuu, nambari ya usajili KCK 583U, lililokuwa limebeba wanafunzi 65 kutoka Shule ya Sanaa na Sayansi ya Jamii, Idara ya Kiswahili, lilihusika katika ajali isiyo ya mauti katika eneo la Kimende kwenye barabara kuu ya Nakuru-Nairobi wakati wa safari ya kimasomo,” alisema Kosgei katika taarifa.

“Kama hatua ya tahadhari, safari zote za kimasomo zimesitishwa hadi baada ya Sikukuu ya Pasaka.”

Kwa bahati nzuri, hakukuwa na majeruhi au vifo vilivyoripotiwa, na wanafunzi wote wako salama. Usafiri mbadala umeandaliwa ili kuwarudisha wanafunzi katika chuoni.

Ajali hii imetokea wiki mbili tu baada ya basi lingine la Chuo Kikuu cha Kenyatta kupata ajali eneo la Voi, Kaunti ya Taita Taveta likielekea Mombasa.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu, Machi 18 baada ya basi la chuo hicho kugongana na trela na kusababisha vifo vya wanafunzi 11. Wengine kadhaa walijeruhiwa wakati wa katika ajali hiyo.