Home Kimataifa Chumba cha matumizi ya dawa haramu za kulevya chaidhinishwa Uingereza

Chumba cha matumizi ya dawa haramu za kulevya chaidhinishwa Uingereza

0

Serikali ya Uingereza imeidhinisha chumba cha kwanza kabisa cha matumizi ya dawa za kulevya zilizoharamishwa zikiwemo heroin na cocaine.

Chumba hicho kimekubaliwa na serikali ya Scotland na kitajengwa kwenye hospitali moja jijini Glasgow dhamira ikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya ziliyoharamishwa.

Watumizi wa dawa hizo za kulevya wataruhusiwa kuyatumia katika chumba hicho chini ya uangalizi wa wahudumu wa afya waliohitimu.

Bodi ya ushirikiano ya Glasgow ambayo inajumuisha wawakilishi wa huduma ya taifa ya afya NHS na viongozi kutoka baraza la jiji waliidhinisha mpango huo kwenye mkutano ulioandaliwa mtandaoni Jumatano asubuhi.

Mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Scotland unatarajiwa kuwa tayari kufikia mwezi Juni mwaka 2024 na utaendelea kwa muda wa miaka mitatu kwa gharama ya pauni milioni 7.

Daktari Saket Priyadarshi, mkurugenzi wa huduma ya kusaidia watumizi wa pombe na dawa za kulevya ya Glasgow alisema kwenye mkutano huo wa Jumatano kwamba mradi huo unatarajiwa kupunguza idadi ya watu wanaojidhuru wakitumia dawa hizo za kulevya na kuwapa fursa ya matibabu.

Wazo hili limekuwa likijadiliwa kwa muda na sasa wakati umewadia wa kulitekeleza baada ya kubainika kwamba watumizi wengi wa dawa za kulevya huzitumia katika maeneo ya wazi ambayo sio salama.

Tayari watumizi 23 wa muda mrefu wa dawa haramu za kulevya wanaendelea kupokea matibabu katika kliniki moja kwenye barabara ya Hunter mashariki mwa mji wa Glasgow ambapo chumba hicho maalumu kitajengwa.

Website | + posts
BBC
+ posts