Home Habari Kuu Chukueni Pasipoti au ziharibiwe, aonya Kindiki

Chukueni Pasipoti au ziharibiwe, aonya Kindiki

Waziri aliyasema hayo alipozindua mpango wa siku 30 wa utoaji kwa haraka pasipoti ambazo hazijachukuliwa kwa wenyewe.

0

Serikali imeonya kuwa itaharibu pasipoti ambazo hazitakuwa zimechukuliwa na wenyewe baada ya kukamilika kwa muda watakaopewa kuzichukuwa.

Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki alisema wenye pasipoti hizo ambazo hazijachukuliwa pia watatozwa faini katika siku zijazo endapo watatuma maombi ya kupewa paspoti.

Waziri aliyasema hayo katika jumba la Nyayo Jijini Nairobi, alipozindua mpango wa siku 30 wa utoaji kwa haraka pasipoti ambazo hazijachukuliwa kwa wenyewe.

Kulingana na Waziri Kindiki, pasipoti 87,574 ziko tayari kuchukuliwa  lakini wenyewe hawajazichukua katika afisi za idara ya uhamiaji kote nchini.

Alisema serikali imechukua hatua ya kuchapisha majina ya waliotuma pasipoti na tarehe ya kuzichukua.

Aidha alisema wale wanaopaswa kuchukua pasipoti zao watafahamishwa kupitia ujumbe mfupi.