Home AFCON 2023 Chui wa Congo wamla tembo na kufuzu nusu fainali ya AFCON

Chui wa Congo wamla tembo na kufuzu nusu fainali ya AFCON

0
Wachezaji wa Congo wakisherehekea bao katika robo fainali ya AFCON dhidi ya Guinea

Chui wa Congo waliandikisha historia baada ya kuititiga Guinea mabao matatu kwa moja na kutinga nusu fainali ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015.

Robo fainali hiyo ya pili ilipigwa Ijumaa usiku katika uga wa Olympique Alassane Ouattara mjini Abidjan, Ivory Coast.

Mohammed Bayo aliwaweka tembo wa Guinea uongozini kunako dakika ya 20 kupitia tuta la penalti, baada ya Chancel Mbemba kumkwatua mshambulizi wa Guinea karibu na lango.

Mbemba alijizoa dakika saba baadaye na kuwanyanyua mashabiki wa Congo kwa goli la kusawazisha, alipofumania mpira uliotemwa na kipa wa Guinea.

Mashabiki wa Congo wakifuatilia ngarambe kati ya timu yao dhidi ya Guinea

Kipindi cha pili, vijana wa kocha Sébastien Desabre walipiga chafya na kuongeza makali ya mashambulizi, huku Yoanne Wissa akitanua uongozi katika dakika ya 65 kupitia penalti.

Zikisalia dakika nane ngoma ikatike, Arthur Masuaku alichonga free kick iliyotua kimiani na kusajili ushindi wa kihistoria ambapo wanawinda kombe la tatu.

Chui hao wa Congo watakabiliana na mshindi wa kwota fainali ya Jumamosi kati ya wenyeji Ivory Coast na Mali katika semi fainali ya Jumatano.