Serikali ya China imekubali kutoa msaada wa vifaa katika vyuo anuwai kote nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 13.
Kutokana na hilo, Rais William Ruto ameagiza kwamba kila eneo bunge nchini liwe na chuo cha mafunzo ya kiufundi kilicho na vifaa vyote hitajika.
Akizungumza kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka 100 ya mafunzo ya kiufundi nchini katika chuo anuwai cha Nyeri leo, Rais alihimiza maeneo bunge kutumia fursa ya usaidizi huo kutoka Uchina kuanzisha vyuo hivyo.
Alisema pia kwamba watu wengi wamekuwa wakijisajili kupokea mafunzo kwenye vyuo anuwai baada ya wengi kugundua umuhimu wa ujuzi wa kazi mbali mbali za mikono na sasa vyuo hivyo vina wanafunzi zaidi ya elfu 350 kote nchini.
Rais amewataka wakenya kuchukulia vyuo anuwai kuwa muhimu kwani vinatoa mchango kwa maendeleo ya ujuzi.
Kwa upande wake waziri wa elimu Ezekiel Machogu alisema vyuo anuwai vina jukumu la kuleta mabadiliko mazuri katika jamii kwa kuwapa vijana fursa ya kujiendeleza maishani.
Ujuzi kutoka kwa vyuo hivyo alisema unasaidia wanaohitimu kuhusika kikamilifu katika nyanja rasmi na zisizo rasmi za uchumi wa nchi hii.