Sandrafelis Chebet na Vincent Mutai, ndio washindi wa mkondo wa kwanza wa mbio za nyika nchini ulioandaliwa Jumamosi katika kaunti ya Machakos.
Chebet wa Police alitwaa ubingwa wa kilomita 10 akizitimka kwa dakika 34, sekunde 2 nukta 6, akifuatwa na Mercy Chepkorir wa Lemotit kwa dakika 35 sekunde 4 nukta 4, wakati Teresa Cheroritich pia kutoka Lemotit akiambulia nafasi ya tatu.
Vincent Mutai wa KDF alishinda mbio za kilomita 10 wanaume akiziparakasa kwa dakika 29, sekunde 39 nukta 1, akifuatwa na Arthunus Kioko wa Machakos kwa dakika 29, sekunde 42 nukta 2, huku Brian Kiptoo wa Police akimaliza wa tatu.
Katika mbio za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Diana Chepkemoi wa Lemotit ameibuka mshindi wa kilomita 6 wasichana kwa dakika 19, sekunde 58 nukta 1, akifuatwa na Sylvia Chelangat wa Kaptagat kwa dakika 20, sekunde 11 nukta 3, huku Florence Chepkoech wa Lemotit akimaliza wa tatu.
Katika mbio za kilomita 8 wavulana, Clinton Kimutai kutoka Keringet ametwaa ushindi akitumia muda wa dakika 23, sekunde 20 nukta 6 kufika utepeni, akifuatwa na Vincent Kibet wa Nakuru kwa dakika 23, sekunde 48 nukta 7 wakati Shadrack Kemboi wa Nakuru akiridhia nafasi ya tatu.
Mkondo wa pili utaandaliwa Oktoba 21 mjini Kapsokwony na ule wa tatu uandaliwe Sotik tarehe 4 mwezi ujao.