Msanii wa Uganda Joseph Mayanja almaarufu Jose Chameleone amekuwa nchini Kenya ambapo alikuja kwa ajili ya onyesho lake mjini Naivasha la jana Jumamosi.
Akihojiwa kwenye kituo kimoja cha redio kabla ya onyesho hilo, Chameleone alielezea kwamba hadithi aliyotoa kupitia wimbo “Jamila” ni ya ukweli.
Kulingana naye, Jamila ni binti waliyesoma naye shule ya msingi na ambaye alikuwa rafiki wa karibu. Baada ya masomo ya shule ya msingi wakapoteleana hadi walipokutana akiwa msanii nchini Uingereza.
Chameleone anasema Jamila alikuwa mrembo na mwenye hela nyingi wakati huo na alikuwa akiishi nchini Afrika Kusini na mume wake, Uingereza alikuwa amekwenda kutembea.
Jamila ndiposa akaahidi kwamba angemwalika Chameleone nchini Afrika Kusini ili wajadiliane zaidi.
Lakini kila mara Jose alipokuwa akijaribu kuwasiliana naye hakufaulu asijue tatizo. Siku kadhaa baadaye akakutana na kaka ya Jamila nyumbani Uganda akamuuliza aliko akamjuza kwamba alikuwa amefariki.
Kakake Jamila aliendelea kumhadhithia kilichomtokea na baada ya hapo akaamua kumkumbuka rafiki yake kupitia wimbo huo Jamila.
Jose Chameleone ni mmoja wa wasanii wa zamani ambao bado wana ushawishi katika tasnia ya burudani huku wengi walioanza naye enzi hizo wakiwa wamesusia muziki.
Aliwahi kuwa kwenye kundi moja la muziki la wasanii wa Kenya na Uganda almaarufu “East African Bashment Crew”. Wakenya kwenye kundi hilo walikuwa Kevin Wyre na Nazizi na msanii wa Uganda Bebe Cool.