Home Habari Kuu Chama cha ODM chazuiwa kumtimua mbunge wa Gem

Chama cha ODM chazuiwa kumtimua mbunge wa Gem

0

Mahakama ya kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa nchini imesimamisha kwa muda hatua ya chama cha ODM ya kumfurusha mbunge wa Gem Elisha Odhiambo.

Maagizo kutoka kwa mwenyekiti wa mahakama hiyo Desmas Nungo, yanazuia chama cha ODM kisimfurushe Odhiambo hadi pale ambapo kesi aliyowasilisha ya kupinga kufurushwa kwake itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Chama hicho pia kimezuiwa kisichukue hatua ya kumwondoa mbunge huyo kwenye kamati mbalimbali alizoteuliwa kuhudumu bungeni kwa sababu ya kuwa mwanachama wa ODM.

Msajili wa vyama vya kisiasa pia amezuiwa asichukue hatua yoyote katika kutekeleza uamuzi wa chama cha ODM wa kumfurusha Odhiambo.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 20, 2023.

Elisha ni mmoja wa wabunge wa chama cha ODM waliofurushwa wiki jana kwa kile ambacho kinasemekana kuwa kuasi maazimio ya chama chao na kupendelea maazimio ya chama tawala.

Wengine ni Gideon Ochanda wa Bondo, Phelix Odiwuor wa Lang’ata, Caroli Omondi wa Suba Kusini na seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Uamuzi wa kufurusha wabunge hao ulitangazwa na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye alisisitiza kwamba chama hicho hakitakubalia wanachama wasio waaminifu.

Alisema uaminifu kwa chama ni mojawapo ya vitu ambavyo vitafanya chama kikue.