Home Kimataifa Chama cha kuwanufaisha wanawake kiuchumi chazinduliwa Nyanza

Chama cha kuwanufaisha wanawake kiuchumi chazinduliwa Nyanza

Kulingana na Owalo, chama hicho kitatoa mwongozo kuwasaidia wanawake mashinani kuanzisha biashara na kuwaunganisha na wafadhili pamoja na soko.

0
Waziri Eliud Owalo azindua chama cha wanawake wataalam eneo la Nyanza.
kra

Wanawake walio katika  taaluma eneo la Nyaza wamehimizwa kuwa kielelezo na kuwawezesha wanawake kuwa na fursa sawa katika maendelo ya uchumi wa taifa hili.

Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali Eliud Owalo, aliyasema hayo siku ya Ijumaa katika kaunti ya Kisumu, alipozindua chama cha wanawake wataalam katika eneo la Nyanza (PANY).

kra

“Wanawake hawa wataalam katika eneo hili, wanasema wakati wa kulalamika umepita na sasa ni wakati wa kuzungumza kuhusu maendeleo pamoja na kuinua uchumi wa eneo la Nyanza,” alisema waziri Owalo.

Kulingana na Owalo, chama hicho kitatoa mwongozo kuwasaidia wanawake mashinani kuanzisha biashara na kuwaunganisha na wafadhili pamoja na soko.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama hicho cha PANY Betty Adera, alisema chama hicho ambacho kilianzishwa mwezi Februari mwaka 2023, kinanuia kuwaimarisha kiuchumi wanawake walio katika taaluma na kuendeleza eneo la Nyanza.

“Chama hiki kimegundua kwamba mchango wa wanawake walio katika taaluma katika maenedeleo ya kanda hii ni haba, ikizingatiwa kuwa iwapo wanawake watatekeleza jukumu kubwa katika jamii, wataleta udhabiti wa kiuchumi na kijamii na kukuza maendeleo ya muda mrefu,” alidokeza Adera.

Hadi kufikia sasa zaidi ya wanawake 500 walio katika taaluma katika eneo la Nyanza, wamejiunga na chama hicho. Wanawake hao wanatoka katika taaluma za afya, elimu, sheria na biashara miongoni mwa taaluma zingine.

Website | + posts