Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) wa chama cha Jubilee sasa utaandaliwa Agosti 7 katika ukumbi wa Bomas of Kenya.
Tangazo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Kanini Kega.
Mrengo wa chama cha Jubilee unaoongozwa na Kega awali ulikuwa umeitisha mkutano huo Julai 22.
Hata hivyo, mkutano huo ulizuiwa na Jopo la Kusuluhisha Migogoro ya Vyama vya Kisiasa, ORPP hadi kesi iliyokuwa imewasilishwa na mrengo wa mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni isikilizwe na kuamuliwa.
Jopo hilo limemthibitisha Kanini Kega kuwa Katribu Mkuu wa chama cha Jubilee katika hatua ambayo wengi walitazamia itasaidia kutuliza joto la kisiasa chamani.
Hata hivyo, Kioni ameashiria kuwa ataelekea katika mahakama kuu kupinga uamuzi wa ORPP wa kutambua Kega na wenzake kuwa maafisa halali wa chama hicho.
Mrengo wa Kioni uliandaa Mkutano wake wa Kitaifa wa Wajumbe mnamo mwezi Mei, mkutano ambao ulihudhuriwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Wakati wa mkutano huo, maafisa 12 wa mrengo wa Kega walifurushwa chamani na viongozi wapya kuteuliwa.
Hata hivyo, mrengo wa Kega uliwafurusha Kioni na David Murathe chamani na kutangaza kuteuliwa kwa maafisa wapya huku aliyekuwa mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Murang’a Sabina Chege akitangazwa kuwa kiongozi wa chama.
Uamuzi wa jopo la kusuluhisha migogoro ya kisiasa unamaanisha mrengo wa Jubilee unaoegemea upande wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta sasa umeachwa katika njia panda baada ya kunyang’anywa chama walichokipigania kwa udi na uvumba.