Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kitaandaa chaguzi zake kuanzia Aprili 27, 2024.
Katika mkutano na wanahabari leo Jumatano, chama hicho kilisema usajili wa wanachama utaendelea kote nchini, kwa maandalizi ya chaguzi za nyanjani na kitaifa.
Chaguzi hizo zinatarajiwa kuandaliwa katika kaunti tisa, ambapo katika kaunti za Kwale, Busia na Siaya chaguzi hizo zitaandaliwa Aprili, 27 huku katika kaunti za Kajiado, Migori na Wajir zikiandaliwa Aprili 29, nazo kaunti za Kisii, Vihiga na Murang’a zikiandaa chaguzi zao Aprili 30.
Katibu Mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna, alisema chama hicho pia kimeandaa mkutano wa kamati kuu ya kitaifa NEC, April 11, kuidhinisha kamati tekelezi ya kitaifa, itakayosimamia zoezi hilo.
Sifuna ambaye alisoma taarifa ya chama hicho katika afisi ya Capitol Hill, alisema chama hicho kitachapisha ratiba ya chaguzi hizo katika kaunti 38 ambazo zimesalia.
“Ratiba ya chaguzi katika kaunti zilizosalia itatolewa. Tumekubaliana kuendelea na zoezi la usajili wa wanachama, huku tukijiandaa kwa chaguzi za nyanjani na kitaifa,” alisema Sifuna.
Aidha katibu huyo mkuu alionya kuwa, chaguzi hizo hazipaswi kuwagawanya wanachama.
“Tulikubaliana kuwa tusikubali chaguzi hizo kuwa chanzo cha migawanyiko na mianya katika chama cha ODM,” aliongeza Sifuna.