Ugumu wa maisha unaotokana na kupanda kwa gharama za maisha sambamba na mabadiliko cha sheria za uchaguzi umeteka maandamano ya chama kikuu cha Upinzani Tanzania, Chadema.
Maandamano hayo yalianza leo jijini Dar es Salaam, ambapo Chadema ilikuwa na hoja tatu kuu huku ikieleza kuwa itaendelea na maandamani katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Hoja hizo kuu ilikuwa ni kutaka katiba mpya, mabadiliko ya miswada ya Sheria za uchaguzi na kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, maandamano hayo yaliyokuwa yameanzia kwenye maeneo mawili tofauti yaani Buguruni na Mbezi mwisho yalitamatia katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) zilizopo katika eneo la Ubungo ambapo chama hicho kiliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa zikieleza kuwa barua hiyo inabeba yote wanayopitia watanzania.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema yalikuwa ni maandamano ya amani na yataendelea katika mikoa mingine mapaka pale yatakapotokea mabadiliko.
Mbowe alisema, ”Tumefanya maandamano makubwa na marefu bila mtu kuumizwa, na hiyo ndio tabia Chadema. Pale polisi wanapoelewa hoja zetu hatuna ugomvi na mtu. Tutaendelea kuandamana katika taratibu na mikoa mbalimbali mpaka wenzetu watuelewe tunamaamisha nini.”
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro alisema kuwa jeshi hilo halijaona kasoro isipokuwa watafanya tathmini ya kiusalam ya maandamano hayo.
”Sisi jeshi la polisi, ushiriki wetu ulikuwa ni kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa sheria havifanyiki. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha kila kitu kiko salama. Tutafanya tathmini ya maandamano hayo.”