Home Habari Kuu Bwawa la Karimenu kaunti ya Kiambu limejaa pomoni

Bwawa la Karimenu kaunti ya Kiambu limejaa pomoni

Hata hivyo shirika hilo la maji la Athi, kupitia ukurasa wake wa twitter, limedokeza kuwa wananchi hawataathiriwa na maji hayo yanayotiririka kutokana na muundo dhabiti wa bwawa hilo.

0
Bwawa la Karimenu kaunti ya Kiambu.

Shirika la ustawishaji maji la Athi limetangaza kuwa mvua kubwa inayoshuhudiwa hapa nchini, imesababisha bwawa la Karimenu II lililoko Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, kujaa na maji ya ziada yameanza kutiririka.

Hata hivyo shirika hilo la maji la Athi kupitia ukurasa wake wa twitter, limedokeza kuwa wananchi hawataathiriwa na maji hayo yanayotiririka kutokana na muundo dhabiti wa bwawa hilo.

“Muundo wa bwawa hilo unauwezo wa kudhibiti maji ya mafuriko na sehemu za kupitishia maji ni salama kwa maeneo ya chini, dhidi ya mvua za El Nino,” lilisema shirika hilo.

Aidha shirika hilo limethibitisha kuwa limechukua hatua za dharura za kuzuia madhara yoyote.

Haya yanajiri huku waziri wa kawi Davis Chirchir akidokeza kuwa bwawa la Masinga huenda likafurika, kutokana na mvua inayonyesha hapa nchini.

Waziri Chrichir aliwasihi wanaoishi karibu na bwawa hilo kuhamia maeneo salama, ili kuepusha maafa na kupunguza uharibifu wa mali.

Taifa hili linashuhudia msimu wa mvua unaosababishwa na hali ya El Nino.