Home Habari Kuu Bunge laidhinisha uteuzi wa Andrew Mukite Musangi

Bunge laidhinisha uteuzi wa Andrew Mukite Musangi

0
Andrew Mukite Musangi

Bunge la taifa limeidhinisha uteuzi wa Andrew Mukite Musangi kama mwenyekiti wa bodi ya benki kuu ya Kenya.

Mjadala wa kutafuta kuidhinisha uteuzi wake, uliwasilishwa bungeni na mbunge wa eneo bunge la Molo Francis Kuria Kimani ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu fedha na mipango ya kitaifa.

Kamati hiyo pamoja na ile ya seneti kuhusu fedha na bajeti, zilimpiga msasa Musangi katika kikao cha pamoja na kulingana na Kimani, kamati izo ziliridhika na wasifu wake.

Musangi aliahidi kamati hiyo ya pamoja ya bunge la taifa na lile la seneti kwamba atahakikisha usimamizi bora wa benki kuu, atahakikisha maandalizi na matumizi ya sarafu ya kwanza ya Kenya ya mitandaoni, aboreshe kitengo cha uchunguzi wa ulaghai katika benki ya kibiashara ili kulinda fedha za wateja na kuendeleza azima ya maandalizi ya sarafu moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Musangi anachukua mahali pa Mohamed Nyaoga ambaye muhula wake wa kuhudumu ulifikia kikomo kwa wakati mmoja na muhula wa aliyekuwa gavana wa benki kuu Patrick Njoroge.

Rais william Ruto alitangaza uteuzi wa Musangi Agosti 17, 2023 na kuwasilisha jina lake bungeni kwa usaili kabla ya kuidhinishwa.

Musangi amekuwa akihudumu kama mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Centum Investment Company Limited.

Website | + posts