Bunge la kitaifa limepitisha hoja ya kuondolewa afisini kwa waziri wa kilimo na ufugaji Mithika Linturi. Hii ni baada ya wabunge 149 kuunga mkono hoja hiyo baada ya mjadala.
Katika kikao hicho cha Alhamisi asubuhi, wabunge 33 walipinga kuondolewa afisini kwa Linturi huku wengine watatu wakikosa kupigia kura hoja hiyo.
Kufuatia hatua hiyo, kamati ya wanachama 11 itabuniwa ili kuchunguza malalamishi dhidi ya waziri Linturi na kuwasilisha ripoti bungeni katika muda wa siku 10.
Hoja ya kuondolewa afisini kwa waziri huyo ilifikishwa bungeni na mbunge wa Bumula Jack Wamboka, ambaye anataka Linturi aondolewe afisini kwa sababu tatu ambazo ni ukiukaji wa katiba, ukiukaji wa kifungu nambari 46 cha katiba na ukiukaji wa maadili.
Hatua hii inatokana na usambazaji wa mbolea gushi kwa wakulima chini ya mpango wa serikali kuu wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima kote nchini.