Home Habari Kuu Bunge la Taifa labuni kamati ya pamoja kuchunguza shughuli za Worldcoin

Bunge la Taifa labuni kamati ya pamoja kuchunguza shughuli za Worldcoin

0

Bunge la Taifa limebuni kamati ya pamoja ya wabunge 15 itakayochunguza shughuli za kampuni ya Worldcoin humu nchini. 

Spika Moses Wetang’ula anasema kamati hiyo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake Septemba 28, 2023.

Kamati hiyo itajumuisha wabunge kutoka kamati za Utawala na Usalama wa Kitaifa, Mawasiliano, Habari na Ubunifu na kamati ya Utalii.

Kampuni ya Worldcoin ilizua gumzo nchini baada ya maelfu ya raia kujitokeza katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC mapema mwezi huu ili kujiandikisha na kampuni hiyo kwa kuchukuliwa data za mboni zao za macho.

Wengi wameelezea mashaka kuhusiana na usalama wa data zilizokusanywa na kampuni hiyo huku wale ambao data zao zilichukuliwa wakilipwa shilingi elfu 7.

Mawaziri Kithure Kindiki wa Usalama wa Taifa na Eliud Owalo wa Habari na Mawasiliano walifika bungeni mapema mwezi huu kuelezea kinagabaubaga wanachokifahamu kuhusiana na shughuli za kampuni hiyo.

Waliwaelezea wabunge kuwa Worldcoin ni kampuni ambayo haijasajiliwa kisheria humu nchini na kwamba serikali imesitisha shughuli za kampuni hiyo inayojihusisha na sarafu ya kidijitali mtandaoni humu nchini huku uchunguzi wa jinai ukianzishwa kubainisha uhalali wa shughuli zake.

Hata hivyo, wabunge hawakuridhika na maelezo yaliyotolewa na mawaziri hao wawili kuhusiana na kampuni ya Worldcoin, hali ambayo imesababisha kubuniwa kwa kamati ya pamoja ya bunge.

Kindiki na Owalo waliokuwa wamepangiwa kufika mbele ya wabunge kwa mara nyingine kesho Jumatano sasa wametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kutoa maelezo zaidi kuhusu Worldcoin punde itakapoanza uchunguzi wake.

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here