Bunge la Taifa litarejelea vikao vyake leo Jumanne baada ya kukamilika kwa mapumziko ya muda mrefu.
Bunge hilo linatarajiwa kushughulikia ripoti ya kamati ya pamoja kuhusu uteuzi wa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.
Usaili wa Kanja ulitekelezwa na kamati ya pamoja kuhusu utawala, maswala ya ndani na ile ya ulinzi, usalama wa taifa na mambo ya nje.
Vile vile, wabunge hao pia watajadili ripoti ya kamati ya pamoja kuhusu uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Ushindani.
Miswada kadhaa imeratibiwa kusomwa kwa mara ya pili, ikiwa ni pamoja na Mswada wa Kahawa (2023) unaolenga kudhibiti sekta ya kahawa kuhakikisha ustawi wake.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ametoa wito kwa kamati inayoshughulika na uratibu wa shughuli za bunge kulipa kipaumbele swala la uundaji upya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka – IEBC.
Wetang’ula alieleza haja ya kuundwa upya kwa tume hiyo haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo unafanywa na mipaka inawekwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.