Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi amesema kwamba bunge la Seneti litabadilisha kalenda yake kufuatia matukio ya jana ambapo waandamanaji waliingia katika majengo ya bunge.
Kulingana na Kingi, mjadala utawasilishwa na kupitishwa katika bunge hilo uratibu tarehe nyingine ya kurejelea vikao.
Maseneta walikuwa wamepangiwa kurejelea vikao vyao jana alasiri baada ya likizo ya muda lakini kikao hicho kikavurugwa na uvamizi wa waandamanaji katika majengo ya bunge.
Waandamanaji waliokuwa wakilalamikia mswada wa fedha wa mwaka 2024 waliingia bungeni na kuvuruga mambo ambapo wengine waliondoka na vifaa kadhaa huku vingine vikiharibiwa.
Taarifa ya Kingi inafuatia mkutano uliofanyika mapema leo wa kamati ya mipango ya bunge la seneti.
Spika huyo alitambua haki ya kila mkenya ya kukusanyika na kufanya maandamano kwa njia ya amani lakini akasisitiza kwamba hilo lazima lifanyike kwa mujibu wa sheria.
Alipongeza maafisa wa usalama kwa kuchukua hatua na kuhakikisha hali ya kawaida inarejea katika majengo ya bunge ingawaje watu kadhaa walipoteza maisha na ametoa risala za rambi rambi kwa ndugu jamaa na marafiki wa waathiriwa.