Home Habari Kuu Bunge la Seneti laidhinisha kubuniwa kwa kamati ya mazungumzo ya pande mbili

Bunge la Seneti laidhinisha kubuniwa kwa kamati ya mazungumzo ya pande mbili

Kamati hiyo iliidhinishwa na bunge la kitaifa wiki iliyopita.

Bunge la Seneti limeidhinisha hoja ya kubuniwa kwa kamati ya mazungumuzo ya kitaifa ya mazungumzo, kutoa fursa ya mazungumzo kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya. 

Kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Aaron Cheruiyot akiwasilisha hoja hiyo, alisema ana imani kwamba suluhu itapatikana kwa maswala yanayoibua utata.

Kiongozi wa wachache katika bunge hilo Steward Madzayo naye aliunga mkono hoja hiyo, akisema ana matumaini kuwa pande zote mbili zitapendekeza mageuzi yanayofaa ya kisheria na sera kuhusu maswala yanayowaathiri Wakenya kuambatana na katiba.

Wakati wa majadiliano bungeni leo Jumanne asubuhi, maseneta wengi pia waliunga mkono hoja ya kubuni kamati hiyo.

Hata hivyo, wachache miongoni mwao akiwemo seneta wa kaunti ya Tana River Danson Mungatana walisema huenda fursa hiyo ikatumiwa vibaya na wanaoshindwa kwenye uchaguzi.

Kupitishwa kwa hoja hiyo kunaipa kamati hiyo inayoongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah mamlaka ya kisheria kupendekeza mageuzi ya katiba na sheria baada ya mazungumzo ya kitaifa kukamilika.

Kamati hiyo iliidhinishwa na bunge la kitaifa wiki iliyopita.

Website | + posts
Radio Taifa
+ posts