Home Habari Kuu Bunge kuandaa kikao cha mabadiliko ya tabia nchi kesho

Bunge kuandaa kikao cha mabadiliko ya tabia nchi kesho

0

Bunge la Kenya litaandaa kikao cha mazungumzo bungeni kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kesho Jumatano, Septemba 6, 2023.

Haya ni kulingana na taarifa ya pamoja ya spika wa bunge la Taifa na spika wa bunge la Seneti.

Wabunge wote wanaohudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi katika jumba la KICC wamealikwa kwa kikao hicho.

Spika wa bunge la Taifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi wataongoza kikao hicho.

Katika taarifa kwa wabunge, maspika hao wawili walisema ni muhimu kwa wabunge kujadili na kukubaliana kuhusu njia za kuimarisha uwezo wa Afrika wa kuathiri kwa njia chanya ajenda ya tabia nchi na kuhimiza ulimwengu kutumia fursa nyingi zilizopo barani Afrika za kuafikia mazingira safi.

Maspika Wetangula na Kingi walielezea kwamba dhamira ya kikao cha kesho ni kukutanisha wabunge wa nchi za Afrika wanaohusika na masuala ya tabia nchi katika mabunge yao, kujadili jukumu la mabunge katika kuafikia matokeo ya kongamano linaloendelea.

Wabunge hao watajadili kuhusu nyanja za kuongeza maarifa kwa wabunge ili kutekeleza uangalizi unaofaa katika utekelezaji wa maazimio ya tabia nchi.

Maspika hao kadhalika walifafanua kwamba kilele cha kikao cha kesho ni kukubali taarifa ya pamoja ya wabunge katika kongamano linaloendelea kuhusu mabadiliko ya tabia nchi katika jumba la KICC, jijini Nairobi.

Website | + posts