Home Kimataifa Bondia Mwakinyo afungiwa kwa mwaka mmoja na TPBR

Bondia Mwakinyo afungiwa kwa mwaka mmoja na TPBR

0

Tume inayosimamia michezo ya ndondi nchini Tanzania – TPBR imetangaza kwamba bondia Hassan Mwakinyo amepigwa marufuku kwa mwaka mmoja na kutozwa faini ya shilingi milioni moja za Tanzania sawa na shilingi elfu 59 za Kenya.

Hii ina maana kwamba hawezi kuhusika kwenye pigano lolote ndani na nje ya Tanzania hadi mwaka mmoja ukamilike.

Adhabu hiyo inatokana na hatua yake ya kukosa kuingia uwanjani kupambana na bondia Julius Indonga wa Namibia Septemba 29, 2023.

Inasemekana Mwakinyo aligoma baada ya promota wake kukiuka baadhi ya makubaliano yao.

Mwakinyo aliwahi kujipata katika hali sawia nchini Uingereza mwaka 2022 alipopigwa marufuku na bodi inayosimamia ndondi nchini Uingereza.

Haya yalijiri muda mfupi baada yake kushindwa na bondia wa Uingereza Liam Smith na bodi hiyo haikutangaza sababu iliyochochea hatua hiyo.

Mwakinyo wa umri wa miaka 28 ambaye jina lake halisi ni Halfan Hythani Hamza, alianza kupigana ndondi akiwa na umri wa miaka 20 alipopigana na Alibaba R Tarimo, Novemba 29, 2015.

Tangu wakati huo, amehusika kwenye mapigano zaidi ya 20 ambapo ameibuka mshindi katika mengi.

Website | + posts