Home Kimataifa Bomu la gari lasababisha vifo sokoni Syria

Bomu la gari lasababisha vifo sokoni Syria

0

Watu wapatao saba wameuawa katika shambulizi la bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari katika soko moja lenye shughuli nyingi kaskazini mwa Syria.

Wengine wengi waliachwa na majeraha kufuatia shambulizi hilo katika mji wa Azaz ulio katika mkoa wa Aleppo karibu na mpaka wa Uturuki.

Haijabainika ni nani alitekeleza shambulizi hilo katika mji unaosimamiwa na wanamgambo wanaopendelea Uturuki wanaopigana dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria.

Wanajeshi wa Uturuki pamoja na washirika wao huwa wanasimamia sehemu nyingi za Syria zilizo karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Shambulizi hilo lilitekelezwa wakati watu wengi walikuwa wamejitokeza kununua mavazi mapya kwa ajili ya Sikukuu ya Eid al-Fitr, inayoashiria mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kundi la uokoaji kwa jina “White Helmets” linalotekeleza shughuli zake nchini Syria lilisema kwamba watoto wawili ni kati ya waliouawa katika shambulizi hilo.

Hakuna kundi ambalo limedai kutekeleza shambulizi hilo.