Home Kimataifa Bohari la mafuta lalipuka Benin na kusababisha vifo

Bohari la mafuta lalipuka Benin na kusababisha vifo

0

Watu wapatao 35 wameangamia baada ya bohari moja haramu la mafuta kulipuka na kushika moto nchini Benin.

Moto huo wa jana Jumamosi, ulitokea kwenye bohari la kuhifadhi mafuta yaliyolanguliwa katika mji wa Seme-Podji karibu na mpaka wa Nigeria, ambapo waendehaji magari na pikipiki hufika kuyanunua.

Katika taarifa, msimamizi wa mashtaka Abdoubaki Adam-Bongle alisema kwamba moto huo uliharibu kabisa bohari hilo na kusababisha vifo vya watu 35 akiwemo mtoto mmoja.

Abdoubaki alisema kwamba shahidi mmoja alisimulia kwamba moto ulizuka wakati wafanyakazi wa bohari hilo walikuwa wakipakua Petroli iliyokuwa imewasilishwa huko.

Watu wengine zaidi ya 12 waliachwa na majeraha mabaya na wanaendelea kupokea matibabu hospitalini.

Video iliyosambazwa mitandaoni inaonyesha moshi mkubwa wa rangi nyeusi na miale ya moto hewani juu ya kile kinachoonekana kuwa soko huku watu wakitizama kwa mshtuko.

Waziri wa mambo ya ndani nchini Benin Alassane Seidou alitaja mafuta yaliyolanguliwa kuwa chanzo cha moto huo. alisema pia kwamba miili ya waathiriwa imeharibika sana.

Ulanguzi wa mafuta ni jambo la kawaida katika mpaka wa mataifa ya Benin na Nigeria ambayo huzalisha kiwango kikubwa cha mafuta.

Website | + posts