Mwanasiasa na mwanamuziki wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameondolewa marufuku ya kusafiri Uingereza.
Habari za kuondolewa kwa marufuku hiyo zilifichuliwa na Wine mwenyewe kupitia mtandao wa X.
Wine ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform – NUP alipigwa marufuku kusafiri nchini Uingereza kutokana na wimbo wake kwa jina “Burn Dem” wa mwaka 2014.
Wimbo huo ulichukuliwa kuwa wa kuhimiza kudhalilishwa kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja au ukipenda mashoga na wasagaji.
“Nina furaha kuwajulisha kwamba marufuku ya kuingia Uingereza dhidi yangu imeondolewa hatimaye na nitazuru Uingereza hivi karibuni baada ya miaka zaidi ya 10.” aliandika Wine kwenye X huku akishukuru mawakili ambao walisaidia kuafikia kuondolewa kwa marufuku dhidi yake.