Home Habari Kuu Bima ya matibabu NHIF kuondolewa

Bima ya matibabu NHIF kuondolewa

0

Bima ya kitaifa ya matibabu NHIF itaondolewa na badala yake kubuniwe hazina tatu za matibabu. Hili lilibainika kwenye mkutano wa baraza la mawaziri uliondaliwa katika ikulu ndogo ya Kakamega, chini ya uenyekiti wa Rais William Ruto.

Hazina ya NHIF ambayo ndiyo nguzo ya msingi ya utekelezaji wa mpango wa huduma bora za afya kwa wote inaondolewa na mahala pake kuchukuliwa na hazina ya huduma msingi za afya, hazina ya kijamii ya huduma za afya na hazina ya dharura na magonjwa sugu.

Mawaziri walikubaliana kuhusu miswada mitatu ya kuharakisha utekelezaji wa mpango wa huduma bora za afya kwa wote ambayo sasa itaelekezwa bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa.

Inajumuisha, mswada wa mwaka 2023 wa huduma msingi za afya, mswada wa mwaka 2023 wa huduma za afya za kidijitali na mswada wa mwaka 2023 wa hazina ya huduma za afya kwa jamii.

Taarifa kutoka kwa baraza la mawaziri ilielezea kwamba hatua hiyo ya hivi punde inalenga kuharakisha utekelezaji wa ahadi ya serikali kwa wakenya ya uwepo wa huduma bora za afya kwa wote kulingana na mpango wa uwezeshaji kiuchumi wa “Bottom Up Economic Transformation Agenda (BETA)”.

Mswada wa huduma za afya za kidijitali unalenga kuziba mianya iliyopo katika mfumo wa afya kidijitali na uhifadhi wa data ili kuwezesha kubuniwa kwa sera za kuongoza utoaji huduma za afya kwa njia ya kidijitali, kupata dawa kupitia mitandao na elimu ya sekta ya afya mtandaoni.

Rais William Ruto yuko makini kuleta mageuzi katika sekta ya afya hasa kwenye bima ya NHIF ili kuhakikisha wanaotoa michango yao kwa hazina hiyo wananufaika.

Website | + posts