Bima mpya ya afya ya SHA itaanza kutekelezwa tarehe mosi mwezi ujao.
Hadi kufikia sasa, Wakenya milioni 1.2 wamejisajili kwa bima hiyo itakayochukua mahali pa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, NHIF huku zoezi la usajili likiendelea kote nchini.
Wanachama milioni 9 wa NHIF watahamia SHA punde baada ya bima hiyo mpya kuanza kutekelezwa.
Wakati wa mkutano uliofanyika jana Jumanne na kuongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Baraza jipya la Mawaziri lilitaarifiwa mipango iliyowekwa kuhakikisha ufanisi katika uzinduzi wa bima hiyo.
Wizara ya Usalama wa Kitaifa imetakiwa kusaidia kufanikisha shughuli inayoendelea ya uandikishaji kwenye bima hiyo na kuuelimisha kuhusu faida ya kujiandikisha kwenye bima hiyo.
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa anasema bima hiyo itazinduliwa na kutekelezwa hatua kwa hatua.
“Tunazindua SHA Oktoba 1, 2024. Ni bima itakayozinduliwa hatua kwa hatua, huku mafao ya bima hiyo yakitolewa kulingana na rasilimali zilizopo,” amesema Dkt. Barasa.
“Tutaendelea kuboresha mfumo huo wakati tukisonga mbele.”