Home Habari Kuu Biden azungumzia hatua ya kujiondoa kwenye uchaguzi

Biden azungumzia hatua ya kujiondoa kwenye uchaguzi

0
kra

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa hotuba ya kwanza tangu alipotangaza kwamba amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Urais na badala yake anamuunga mkono naibu wake Kalama Harris.

Sasa Biden anaelezea kwamba hatua yake ilichochewa na haja ya kuunganisha chama chake na kuokoa demokrasia ya Marekani.

kra

Alitangaza hayo kwenye ujumbe wa video kutoka kwenye afisi yake ya ikulu ya White House ambapo sauti yake ilitoka kwa upole sana akisema wakati ulifika wa kumpitishia mwingine mwenge wa uongozi.

Tangazo la Biden la kujiondoa alilotoa Jumapili lilifuatia shinikizo za wahusika wakuu wa chama cha Democratic baada ya kukosa kufanya vywema kwenye mjadala na mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump.

Kwa maneno yake mwenyewe Biden alisema kwamba anaheshimu sana afisi ya Rais lakini anapenda nchi yake zaidi na kwamba imekuwa heshima kubwa kuhudumu kama Rais.

“Lakini katika kutetea demokrasia, ambayo imetishiwa, nadhani hilo ni muhimu kuliko wadhifa huu.” alisema Biden.

Huku akisema kwamba Marekani inapitia wakati muhimu sana na kwamba miezi michache ijayo itaamua hatima ya Marekani na ulimwengu, Biden aliwaambia wamarekani kwamba kwa sababu wanaamini katika ukweli, heshima, haki na demokrasia hawafai kuchukulia wapinzani kama maadui.

Biden alisema utendakazi wake, uongozi wa Marekani ulimwenguni na maono yake kwa Marekani ni vitu ambavyo vingempa muhula wa pili kama Rais lakini alichagua kuunganisha chama chake ili kushinda kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba,

“Nimeamua kwamba njia nzuri ya kusonga mbele ni kupitisha huu mwenge kwa kizazi kipya. Hiyo ndiyo njia bora ya kuunganisha taifa letu.” Alisema Biden akirejelea uamuzi wake wa kumuunga mkono Kamala Harris kuwania Urais.